OKWI, MAKAMBO LIGI KUU TANZANIA BARA WATIKISA NOTI

KUNA mastaa wengi wa kigeni ambao klabu za Ligi Kuu Bara zimewanasa, lakini mpaka sasa hawajaonyesha shughuli uwanjani kutokana na kukosa vibali vya kazi.
Mbali na mastaa hao, pia kuna makocha na wataalamu wengine wa benchi la ufundi ambao, wanaendelea kuzishuhudia timu zao wakiwa majukwaani hadi hapo watakapokamilisha taratibu hizo.
Lakini wakati wachezaji hao wakiendelea kusugua kusubiri timu zao kukamilisha utaratibu huo, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limeruhusu ongezeko la wachezaji wa kigeni kwenye klabu moja kutoka watano hadi 10 ambao wanaruhusiwa kucheza kwa wakati mmoja.
Msimu mpya wa Ligi Kuu ulianza mwezi uliopita, baadhi ya timu ziliwatumia wachezaji wao wapya wa kigeni baada ya kukamilisha utaratibu wa vibali huku timu nyingine zikishindwa kuwatumia nyota hao kwani hawajakamilisha utaratibu huo.
Kwa mujibu wa sheria za Tanzania, mtu yeyote ambaye sio raia wa Tanzania, haruhusiwi kufanya kazi ama kuishi kwenye ardhi hii bila kuwa na vibali, iwe cha kazi au cha kuishi.
Vibali vya kazi hutolewa na Wizara ya Kazi wakati vibali vya makazi hutolewa na Idara ya Uhamiaji na ikumbukwe vibali vyote viwili vinakwenda pamoja.
Hata hivyo, kutokana na wachezaji kadhaa kukwama kuanza kutumikia vibarua vyao kwenye klabu hizo huku wakivuta mishahara minono, Mwanaspoti limefuatilia na kubaini mambo mazito kwenye ishu nzima kuanzia Wizara ya Kazi na Ajira, Uhamiaji na TFF yenyewe ambayo imekuwa ikipiga pesa ndefu kutokana na ongezeko la wachezaji wa kigeni.
WAGENI 43
Kwa msimu huu pekee, kuna wachezaji, wataalamu wa benchi la ufundi na makocha ambao wameajiriwa na timu mbalimbali kwa ajili ya msimu wa Ligi Kuu Bara kwa 2018/19.
Lakini kwa ujumla idadi ya wachezaji wa kigeni na makocha waliopo kwenye Ligi Kuu Bara kwa sasa ni 58, ambapo wote wanatakiwa kulipiwa vibali vya kazi na ukazi pamoja na ada nyingine za TFF kwa mwaka.
TFF – SH86 MIL
Kwa taratibu za TFF, kila mchezaji wa kigeni anapaswa kulipiwa ada ya Sh2 milioni kwa mwaka, ambapo fedha hizo huingia kwa TFF. Ada hiyo hulipwa kila mwaka ndipo mchezaji kupata leseni na utaratibu mwingine unaosimamiwa na mamlaka nyingine kama Uhamiaji na Idara ya Kazi.
Awali, kabla ya uongozi wa Rais wa TFF, Wallace Karia, TFF ilikuwa ikitoza Dola za Marekani 2,000 (Sh 4.5 milioni) kila mwaka, lakini msimu huu leseni inalipiwa Sh2 milioni.
Kutokana na kanuni hiyo, msimu huu TFF inavuna Sh 86 milioni kwa mwaka ikiwa ni malipo ya leseni kutoka klabu za Ligi Kuu kwa ajili ya wachezaji wa kigeni 43.
UHAMIAJI - Sh 127 milioni
Ili mchezaji ama kocha aweze kufanya kazi nchini, ni lazima mwajiri wake afuate utaratibu wa kisheria ikiwemo kumlipia kibali cha kazi, makazi na ada ya TFF.
Uhamiaji ni kitengo cha mwisho kutoa kibali cha makazi iwapo mchezaji ama kocha amekamilisha utaratibu wa kupata kibali cha kazi kupitia Wizara ya Kazi na leseni ya TFF.
Gharama za kulipia vibali vya makazi kwa mgeni bila kujali ni mchezaji au kocha ni Dola za Marekani 550 (Sh 1.2 milioni) kwa wale ambao wametoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki ambazo ni Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda.
Kwa mgeni anayetoka nje ya nchi ambazo sio wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki hulipa Dola 2050 (zaidi ya Sh4 milioni).
Makocha wageni wanaotoka ndani ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki waliopo kwenye timu za Ligi Kuu ni 16 ambao, wanaifanya Idara ya Uhamiaji kuvuna Dola 8,800 (zaidi ya Sh 20 milioni) kwa mwaka huku wale ambao sio raia wa nchi wanachama ni 27 waliolazimika kila mmoja kulipiwa Dola 2050 kwa ajili ya kibali cha kuishi nchini.
Vibali hivyo vya kuishi nchini kwa wageni ambao sio raia wa nchi zilizopo Afrika Mashariki, ndivyo vinaonekana kuzikwangua klabu mkwanja mkubwa kwani, jumla wapo wageni 27 wenye sifa hizo ambao huifanya Idara ya Uhamiaji kukusanya Dola 55,350 (zaidi ya Sh 126 milioni).
Fedha zinazokusanywa na Idara ya Uhamiaji kwa ajili ya vibali vya kuishi nchini kwa makocha na wachezaji kigeni, kwa jumla ni Dola 64,150 ambazo ni zaidi ya Sh 130 milioni.
Mwanaspoti limezungumza na Mrakibu Mkuu na Msemaji wa Uhamiaji, Ally Mtanda ambaye alielezea jinsi wanavyotoa vibali hivyo ili wageni wapate kuishi na kufanya kazi nchini.
“Kwanza watu wafahamu Uhamiaji hutoa vibali vya makazi tu, lakini vibali vya kazi hutolewa na Wizara ya Kazi, kwetu ni idara ya mwisho kabisa baada ya utaratibu kwa maeneo mengine kukamilika.
“Kuna aina tatu za vibali. Kuna A, B na C mara nyingi A hutumika kwa wawekezaji, B ni kwa waajiriwa ambapo, hapa huingia wachezaji na makocha ama watu wanaokuja kufanya kazi kwenye kampuni mbalimbali.
“Pia, ili mtu apewe kibali hicho ni lazima Uhamiaji wapewe taarifa za kuwaombea vibali hivyo kutoka Wizara ya Kazi, yaani wakiwapa vibali vya kazi hutuma taarifa kwetu.
“Kwa sasa bado hatujapata maombi yoyote kutoka Wizara ya Kazi hivyo, hakuna kibali cha makazi kilichotolewa, bado kuna muda kwani huwa tunatoa muda wa miezi mitatu tangu dirisha la usajili linapofungwa kwa wachezaji.
“Nadhani bado wanaendelea na taratibu za kukamilisha vibali vya kazi ili wapate vya makazi ingawa asipopata kibali cha kazi huyo mchezaji ama kocha hawezi kufanya kazi kwa mujibu wa sheria zetu za nchi.
“Huwa wanapewa vibali vya muda mfupi vya ‘Business Visa’ ambacho kinamruhusu kukaa nchini kwa miezi mitatu wakati anasubiri kushughulikia taratibu za vibali vya kazi.
“Kibali hiki ni kwa wale wanaotoka nje ya nchi za Afrika Mashariki na hulipia Dola 200 wakati wale wa Afrika Mashariki wanapewa kibali cha matembezi (visitors pass) kinacholipiwa Dola 100.
“Mchezaji ama kocha akishindwa kukamilisha utaratibu wa kupata kibali cha kazi anapewa kibali cha kurekebisha hadhi yake ya ukazi ambacho gharama yake ni Dola 600 ama anarudishwa nchini kwao hadi hapo waajiri wake wakimaliza kila kitu,” alisema Mtanda.
Mtanda aliongeza vibali hivyo hulipiwa kwa miaka miwili huku akisisitiza wageni wote kufuata utaratibu wa nchi na sheria zake zinavyoelekeza.
“Miaka ya nyuma tulikuwa tunapata shida kuwabaini watu wanaofanya kazi nchini kinyume na utaratibu, hasa kwa hawa wachezaji mikoa ya Kanda ya Ziwa ambapo wengi hutoka nchi jirani, lakini tunawafuatilia kwa ukaribu ili kila mmoja awajibike kuheshimu na kufuata sheria za nchi.
“Hakuna mgeni ambaye anacheleweshewa kibali chake kama amefuata utaratibu. Wizara ya Kazi wana utaratibu wao na hata uhamiaji kwani, tunapoletewa majina ya watu wanaoombewa vibali ni lazima tuyachunguze kukwepa kuingiza wahaini ama wauza unga na madawa mengine ya kulevya, hata matendo ya kuhatarisha amani ya nchi,” alisema Mtanda.
MAMBO MTANDAONI
Unaweza ukadhani kwamba ni TFF na Idara ya Uhamiaji ndio taasisi pekee zinazonufaika na faida za moja kwa moja kutokana na ujio wa wachezaji wa kigeni, lakini kumbe zipo nyingine ambazo nazo zinavuna pesa ndefu kwa wageni hao.
Wizara ya Kazi nayo inaneemeka kutokana na uwepo wa wachezaji wa kigeni kutokana na tozo ambayo imekuwa ikikusanywa ili kuwapa vibali vya kazi wachezaji na makocha hao.
Kiasi cha tozo kwa mgeni ili afanye kazi nchini ni Dola 1,000 kwa kila mtu na kwa msimu huu tu, sura mpya za kigeni zilizoongezeka kwenye timu mbalimbali zimeifanya wizara hiyo kuvuna Dola 39,000 (zaidi ya Sh 88 milioni).
Hata hivyo, pamoja na wizara hiyo kuvuna fedha kutoka kwa wageni wanaotua nchini kuzitumikia klabu mbalimbali, bado vibali hivyo havitoki kirahisi.
Hali hiyo imesababisha baadhi ya wachezaji na makocha kucheleweshewa vibali vyao jambo ambalo limekuwa likisababisha wachelewe kuzitumikia timu zao.
Hivi karibuni kumekuwepo na malalamiko kwa baadhi ya viongozi wa klabu kupata changamoto kwenye suala la kuomba vibali.
Vibali havitoki kwa muda na wengine hushindwa kuwatumia wachezaji wao. Naibu Waziri wa Kazi, Antony Mavunde anafafanua hilo.
“Kwa sasa tupo kwenye hatua za mwisho kukamilisha mfumo mpya wa kuomba vibali kwa watu wote, kila mwajiri ataomba vibali vya kazi kwa wafanyakazi wake wa kigeni kwa njia ya mtandao. Watajibiwa maombi yao kwa njia ya mtandao yaani kila kitu kitawekwa wazi.
“Kuchelewa kupata vibali hutokana na waombaji wenyewe ambapo baadhi hutumia njia ambayo sio sahihi, kushindwa kukamilisha nyaraka kwa wakati. Kawaida huchukuwa siku 14 mwombaji anakuwa amepewa majibu ya kukubaliwa ama vinginevyo, kwani kuna utaratibu pia wanafuata ili tutoe hivyo vibali.
“Huo mfumo ukianza utarahisisha kila kitu maana fomu zote za maombi zitapatikana huko na watajaza huko huko mtandaoni, kikubwa wakidhi vigezo na wasipitie kwa mawakala kuomba vibali, hapo ndio wanachelewa.
“Kila klabu inapaswa kuomba yenyewe. Kibali cha makazi kinatolewa na Uhamiaji ambao sasa tufanyakazi kwa ushirikiano mkubwa.
“Tunatamani watu wengi waje kufanyakazi nchini, kwani inaleta changamoto na pia uchumi wa nchi unapanda ambapo, kila kibali haijalishi mtu anatoka nchi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ama kwingine ni lazima alipe Dola 1,000 na anapata kibali cha kazi kwa kipindi cha kuanzia mwaka mmoja na haizidi miaka miwili,” alisema Mavunde.
Simba, Yanga, Azam maumivu zaidi
Kama kuna klabu ambazo zinatumia fedha nyingi kulipia vibali vya wageni ili wazitumikie, klabu vigogo vya soka Yanga, Azam na Simba ndizo zinagharamika zaidi.
Tabia ya timu hizo kuajiri kundi kubwa la wacheaji na makocha kutoka nje ya nchi, imezifanya zikutane na mzigo mkubwa wa gharama ambao zinalazimika kulipa ili wageni wao wacheze.
Tathmini iliyofanywa na Mwanaspoti, imebaini kwa msimu huu tu, Simba imetumia Sh 49.3 milioni kulipia vibali vyote vya wageni wake, ikifuatiwa na Azam FC (Sh 41.8 milioni) huku Yanga ikishika nafasi ya tatu kwa kutumia Sh 41. 3 milioni.
Mbeya City yenyewe ndio inayotumia kiasi kidogo zaidi cha fedha kugharamia vibali vya wageni waliopo kwenye kikosi chake, ambapo inalipa Sh 5.5 milioni kwa ajili ya kocha wake, Ramadhani Nsanzurwimo na kipa Owen Chaima.
Simba yenyewe ina wachezaji tisa wakiwemo waliosajiliwa msimu huu na wale wa zamani, Azam ina wachezaji saba, Yanga (5), Singida United (5), Stand United (4), Mwadui FC (4) na Biashara United yenye wachezaji wanne pia.
KMC ambayo imepanda daraja msimu huu, ina wachezaji watatu wa kigeni, Alliance na African Lyon wao wana wawili wawili huku Mbeya City ikiwa na mmoja.
Ukichana na wachezaji, baadhi ya timu zimeajiri wataalamu wa benchi la ufundi wa kigeni ambapo timu za Simba, Yanga, Azam, Stand Unted, Mwadui FC, KMC, Mbeya City na Biashara United zimeajiri makocha wa kigeni.
MAAJABU YA BIASHARA UNITED
Katika hali ya kushangaza licha ya ugeni wake kwenye ligi na ikionekana haina vyanzo vingi vya mapato kama ilivyo kwa Simba, Azam na Yanga, timu ya Biashara United imeingia kwenye kundi la klabu zinazotoa kiasi kikubwa cha fedha kulipia vibali vya makocha na wachezaji wa kigeni.
Timu hiyo kutoka mkoani Mara, inashika nafasi ya nne nyuma ya Simba, Azam na Yanga kwa kugharamia vibali vya wageni ambapo imetumia Sh 39.3 kwa ajili ya kocha wake, Therry Hitimana. Pia, ina wachezaji wanne iliowanasa kutoka nje, Barola Nourdine, Nkourouma Wilfred, Austine Amos na Alex Francis.

LihatTutupKomentar