SIMBA SC HAIKAMATIKI TPL

Mabingwa watetezi wa Ligi kuu soka Tanzania bara, Simba Sports Club leo wameendeleza ubabe wao katika kampeni ya kutetea ubingwa wao baada ya kuichapa wagonga nyundo, Mbeya City mabao 2-0 katika mtanange uliopigwa kwenye uwanja wa Taifa. 

Goli la dakika ya 11 na lile la dakika ya 45 kutoka kwa straika mpya klabuni hapo, Meddie Kagere ndiyo yaliyoihakikishia Simba ya Uturuki uhakika wa pointi tatu na hivyo kufikisha alama sita baada ya ushindi ule wa bao 1-0 katika mchezo wa ufunguzi dhidi ya Prisons. 

Baada ya kuingia kambani mara mbili, Kagere amefikisha jumla ya mabao matatu ndani ya mechi mbili baada ya kufunga pia katika mchezo uliopita. 

Ushindi huo unaifanya Simba kufikisha jumla ya alama 6 ikishinda mechi zote ambapo Mbeya City bado haina alama zozote mpaka sasa kutokana na kupoteza mchezo wake wa kwanza dhidi ya Azam FC. 

Simba sasa wanajiandaa kukabiliana na Lipuli FC ya Iringa katika mchezo utakaopigwa katika dimba la Taifa.

LihatTutupKomentar