KAGERE WA SIMBA, YANGA ASINGEUZWA.

Na MOSES FRANCIS
0743243120
John Raphael Bocco ndio mchezaji bora wa msimu uliopita. Bocco aliibeba Simba mabegani pamoja na pacha mwenzake Emmanuel Okwi msimu uliopita wa ligi kuu Tanzania bara. Baadae Simba ikabeba ubingwa baada ya kuwa imepita misimu mitano bila ya taji hilo. Hapo kuna kitu cha kujifunza kwa hizi timu zetu za kariakoo. Pamekuwepo na mawakala ambao wamekuwa  wakiwafuatilia wachezaji wa Tanzania na kuna baadhi ya wachezaji huwa wanatakiwa na hizi timu za nje. Hapo ndipo panapoibuka mambo ya ajabu ajabu. Simba na Yanga huwa zinagoma kuwauza wachezaji wao nyota kwenda timu za nje zikidai kuwa zina mipango nao.
Ni kweli maranyingi wachezaji nyota hubakia kuwa na msaada katika timu zao kwa maana ya kucheza na kunipa timu zao matokeo. Lakini hapo hapo twende mbele turudi nyuma kuwa mpira ni biashara yenye pesa nyingi na faida kubwa. Wenzetu ulaya nadhani wamefika hapo walipo kwa sababu wanatambua umuhimu wa kuwekeza kwenye soka kama watu wanavyowekeza kwenye sekta nyingine. Timu nyingi za ulaya pale zinapopata ofa kubwa hasa kwa wachezaji wao nyota wachezaji hao hapo hapo huwa wanauzwa. Wachezaji wengi ulaya hulelewa katika misingi ya weledi ili waje kuwa wachezaji wakubwa na baadae wauzwe kwa pesa nyingi.
Hiyo ndio tafsiri halisi ya weledi katika soka. Ni weledi ambao hata Gor Mahia ya Kenya imeufanya kwa Meddie Kagere ambaye imemuuza kwenda Simba. Katika michuano ya Sports Pesa iliyomalizika siku za hivi karibuni pale Kenya Meddie Kagere alikuwa anafunga magoli anavyotaka. Simba ikaulizia bei yake na Gor Mahia ikatamka pesa wanayotaka Simba ikatoa pesa za Mo' na baadae Kagere akawa ameuzwa. Huo ndio weledi katika soka. Timu nyingi kwa sasa zinatumia muda mwingi kuwalea wachezaji ili badae waje wauzwe na timu zipate pesa na si makombe. Klabu ya Inter milan kwa sasa imemuweka sokoni mshambuliaji waoMarco Icardi. Timu yoyote inayomtaka Icardi kwa sasa inakaribishwa ikazungumze na Inter Milan. Kwa sasa huenda timu za nje zimeulizia upatikanaji wa washambuliaji kama Emmanuel Okwi au John Bocco na huenda timu hizo zimeambiwa kuwa wachezaji hao hawauzwi. Mimi ninaamini na nitaendelea kuamini kuwa kama mshambuliaji Meddie Kagere angekuwa anachezea Simba au Yanga katika michuano ya Sport Pesa kamwe asingeuzwa. Mashabiki wa Simba au Yanga pamoja na viongozi wa timu hizi wangejitokeza kwenye vyombo vya habari na kudai kuwa hauzwi mchezaji popote. Mitazamo pamoja na akili za namna hii ni za kijinga.

LihatTutupKomentar