ARGENTINA YAFUTA MECHI YAKE JERUSALEM

Hatua hiyo inaonekana kusababishwa na shinikizo za kisiasa kuhusu vitendo vya Israel dhidi ya Wapalestina wanaoishi Gaza.
Mshambuliaji wa Argentina Gonzalo Higuain ameambia kituo cha ESPN kwamba mwishowe wamefanya jambo lililo sahihi.
Lakini waziri wa ulinzi wa Israel amesema ilikuwa ni jambo la kusikitisha sana kwamba wachezaji wa Argentina hawakuweza "kuhimili shinikizo kutoka kwa maadui wanaoeneza chuki didi ya Israel."
"hatutabadilisha msimamo wetu juu ya kundi la wafuasi wa magaidi wanaoeneza chuki dhidi ya Wayahudi," Avigdor Lierberman ameandika kwenye Twitter.
Ubalozi wa Israel nchini Argentina umeandika kwenye Twitter kuthibitisha kwamba mechi hiyo baina ya mataifa hayo mawili imefutwa.
Tanzania yajitenga na Trump kuhusu Jerusalem
Trump: Palestina iliikosea heshima Marekani
Jerusalem 'uwe mji mkuu wa Wapalestina'
Taarifa za habari zinasema Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alimpigia simu rais wa Argentina Mauricio Macri katia juhudi za kujaribu kuhakikisha mechi hiyo inaendelea.
Mechi hiyo ilikuwa imepangiwa kuchezewa Jerusalem siku ya Jumamosi.
Habari za kufutwa kwa mechi hiyo zimepokelewa kwa shangwe Gaza, ambapo Wapalestina 120 waliuawa kwa kupigwa risasi na wanajeshi wa Israel wakati wa maandamano majuzi.
Mjini Ramallah katika Ukingo wa Magharibi, shirikisho la soka la Palestina limetoa taarifa kumshukuru nyota wa Argentina Lionel Messi na wenzake kutokana na kufutwa kwa mechi hiyo.
"Maadili ya uchezaji yameshinda leo na kadi nyekundu imeoneshwa kwa Israel kupitia kufutwa kwa mchezo huu," mwenyekiti Jibril Rajoub, amenukuliwa na shirika la habari la Reuters.
Bw Rajoub alikuwa awali ametoa wito kwa wapalestina kuchoma fulana na picha za Messi kama juhudi za kutaka mechi hiyo ifutiliwe mbali.
Alitangaza baadaye kwamba ataandaa kikao na wanahabari Jumatano.
Shirika la Avaaz ambalo pia lilikuwa limeitisha kusitishwa kwa mechi hiyo limesifu hatua hiyo ya "kimaadili na jasiri".
"Hii inadhihirisha kwamba Argentina inafahamu kwamba hakuna jambo lolote la urafiki kuchezea Jerusalem, wakati maili chache kutoka hapo kuna wanajeshi wa Israel walenga shabaha wakiwaua waandamanaji wasio na silaha," alisema Alice Jay, mkurugenzi wa kampeni wa Avaaz.
Israel imejitetea kwa kusema wanajeshi wake waliwafyatulia risasi waandamanaji kujilinda au kuzuia watu waliojaribu kuvuka mpaka na kuingia Israel wakati wa maandamano hayo yaliyoandaliwa na kundi la Hamas, ambalo hutawala Gaza.
Kwa nini mji wa Jerusalem ni mtakatifu?
Mechi hiyo ingekuwa ya mwisho kwa Argentina kabla ya mechi za Kombe la Dunia kuanza wiki ijayo.
Jerusalem ni mji wenye utata.
Israel huuchukua kuwa mji wake mkuu wa milele, ilhali Wapalestina huutazama kama mji mkuu mtarajiwa wa taifa lao litakapoundwa.
Mwezi jana, Rais wa Marekani Donald Trump alihamisha ubalozi wa Marekani kutoka Tel Aviv hadi Jerusalem na kuutambia kuwa mji mkuu wa Israel hatua iliyozua maandamano na kushutumiwa vikali na Wapalestina na mataifa mbalimbali duniani.
LihatTutupKomentar