Beki mpya wa Kagera Sugar, Juma Nyosso ameibuka na kuweka wazi kuwa amerejea katika Ligi Kuu Bara kwa lengo moja tu la kupiga kazi na kuonyesha uwezo wake ambao utaisaidia timu yake hiyo kufanya vizuri katika msimu ujao.
Nyosso amerejea kwenye soka la ushindani baada ya kufungiwa miaka miwili na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) alipokuwa akiichezea Mbeya City.
Nyosso aliyewahi kutamba na Simba, amesema kuwa amerejea na nguvu mpya uwanjani akitoka kwenye kifungo ambapo amejipanga kuonyesha uwezo mkubwa ambao utaisaidia timu yake.
“Napenda niwaambie watu kwamba nimerejea tena katika soka na nimekuwa mpya tofauti na yule wa awali ambapo sasa nimekuja na nguvu mpya ya kuipambania timu yangu ifanye vizuri.
“Nina uhakika mkubwa wa kutamba kwenye ligi msimu ujao kwa sababu bado nina uwezo kuliko hata mabeki wengi waliokuwa wanacheza ligi, kiufupi wengi watarajie kitu kipya kutoka kwangu,” alisema Nyosso.